HOTUBA YA KATIBU MKUU WIZARA YA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA
MICHEZO BIBI SIHABA NKINGA , WAKATI WA
UFUNGUZI WA WARSHA YA MAFUNZO YA UKUSANYAJI TAKWIMU ZA UBUNIFU WA SANAA
NA UTAMADUNI NCHINI TANZANIA, JB BELMONT HOTEL,DAR ES SALAAM, TAREHE 9
JUNI, 2014
--
Ndugu Wanawarsha,
Awali ya yote napenda kutumia fursa hii kutoa
shukrani zangu za dhati kwa kunipatia fursa hii ya kuwa Mgeni Rasmi katika
mafunzo haya mafupi ya ukusanyaji wa takwimu za ubunifu wa sanaa na utamaduni
nchini Tanzania “Mapping Study of
Culture and Creative Industries in EAC” – Tanzania Chapter.
Ndugu Wanawarsha,
Napenda kuwapongeza wale wote waliohusika kwa
maandalizi mazuri ya kazi hii, hasa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki
na Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, wakishirikiana na wataalamu wa
Wizara yangu.
Kutokana na umuhimu wa mafunzo na kazi
itakayofanywa baada ya mafunzo, sina budi kuwapongeza pia watumishi wa Serikali
mliobahatika kuchaguliwa kushiriki kwenye programu hii. Fursa hii hamkupewa kama zawadi, bali
imetokana na kutambua juhudi na kujituma kwenu kazini na raghba yenu ya
kumakinikia masuala yanayohusu utamaduni.
Hivyo, nakuombeni mwendelee na umakinifu wenu wakati wote wa mafunzo na
zoezi la ukusanyaji takwimu.
Tena nyie mna bahati kubwa, kwani mnayo fursa ya
kutumia uzoefu walioupata wanajumuiya wenzetu kutoka Kenya, Uganda na Burundi,
ambako mafunzo na utafiti huu vimeshafanywa.
Hivyo, ni matarajio yangu kwamba nyie mtaitekeleza programu hii ya
mafunzo na ukusanyaji takwimu za ubunifu wa kazi za sanaa na utamaduni kwa
ufanisi mkubwa.
Ndugu Wanawarsha,
Kwa muda mrefu kumekuwepo nchini mwetu na dhana
kuwa pamoja na amali nyingi za sanaa na utamaduni tulizonazo, bado hatujawa na
usahihi wa sindano wa idadi kamili ya amali hizo. Aidha, hatuna taarifa za uhakika wa jinsi
amali hizo zinavyochangia kimapato sio tu kwa wasanii wenyewe, bali pia katika
pato la Taifa. Lengo la programu hii
iliyoasisiwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki ni kupata majawabu kuntu kwa maeneo
yote haya ya uelewa wenye ukakasi kwa nchi zote wanachama wa Jumuiya.
Kwa maneno mengine, zoezi hili la ukusanyaji wa
takwimu za ubunifu wa sanaa na utamaduni litasaidi kwa kiasi kikubwa kujua hali
halisi ya sasa ya amali za utamaduni na mustakabali wake wa baadaye kwenye
uchumi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ndugu Wanawarsha,
Nimeyasema yote haya ili kusisitiza umuhimu wa
warsha yenu na kuwataka washiriki wote, na hasa wakufunzi ama wawezeshaji na
wakurufunzi, yaani nyie mnaofundishwa, kuyachukulia kwa uzito wa juu kabisa
mafunzo haya na programu hii kwa ujumla wake.
Ndugu Wanawarsha,
Baada ya maelezo haya machache,
sasa natamka kwamba warsha ya mafunzo ya ukusanyaji wa takwimu za ubunifu wa
sanaa na utamaduni kwa nchi ya Tanzania
IMEFUNGULIWA RASMI.
|
Post a Comment