Magazetini: Nigeria,Libya na Afrika-bara la Matumaini
Nigeria na kuteuliwa Sanusi Lamido Sanusi kuwa amiri mpya wa jiji la
kaskazni-Kano ,Libya na mzozo wa kisiasa na suala kwanini makampuni ya
Ujerumani yako nyuma barani Afrika ni miongoni mwa mada katika Afrika
wiki hii
Tuanzie na Nigeria ambako serikali ya rais Goodluck Jonathan inazongwa
na matatizo ya kila aina:Baada ya visa vya kigaidi vya Boko
Haram,Jonathan anakabwa na mtihani mwengine,nao ni ule wa aliyekuwa mkuu
wa benki kuu ya Nigeria,Sanusi Lamido Sanusi kugeuka kuwa Amiri,au
kiongozi wa mji mkubwa wenye wakaazi wengi zaidi wa kiislamu nchini
Nigeria-KANO.Die Tageszeitung linaandika kuchaguliwa Sanusi kuwa Amiri
wa Kano ni changamoto kwa Jonathan.Baada ya kusifu mchango wake katika
kuurekebisha mfumo wa benki nchini Nigeria,Die Tageszeitung limelinukuu
jarida la kimarekani la Time Magazine lililomtaja mwanauchumi huyo
mwenye umri wa miaka 52 kuwa miongoni mwa watu mia moja wenye ushawishi
mkubwa zaidi ulimwenguni.Hata hivyo shauku kuhusu madaraka mepya ya
Sanusi si kubwa hivyo.Baada ya kutangazwa amiri tu,mamia ya vijana
waliandamana mjini Kano kupinga uamuzi huo.Wangependelea zaidi kumuona
Sanusi Ado Bayero,mtoto wa kwanza wa kiume akimrithi babaake aliyefariki
ijumaa iliyopita.Maoni hayo linaandika die Tageszeitung yanaungwa mkono
pia na rais Jonathan aliyempokonya Sanusi Lamido Sanusi wadhifa wa
kiongozi wa benki kuu,mwezi february uliopita ,baada ya miaka minne tu
madarakani.Gazeti hilo la mji mkuu linakumbusha jinsi mwanauchumi huyo
alivyokuwa akikosoa uzembe wa serikali katika kupambana na rushwa pamoja
na madai kwamba kampuni ya mafuta ya taifa NNPC imetumia vibaya dala
bilioni 20 za umma.Ni nadra kwa lawama kali kama hizo kutolewa hadharani
nchini Nigeria linaandika die Tageszeitung.Kurejea madarakani kama
mtemi ni pigo kwa rais Jonathan linamaliza kuandika die Tageszeitung
linalofafanua umuhimu wa amiri wa Kano na mfalme wa Sokoto katika
harakati za kisiasa nchini Nigeria.Juhudi za kuleta demokrasia Libya
Vurugu nchini Libya pia zimemulikwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani wiki hii.Lilikuwa gazeti la Frankfurter Allgemeine lililoandika kuhusu kisa cha kulazimishwa na korti ya katiba ajiuzulu waziri mkuu Ahmad Maitig.Angalao kwa sasa vurugu za kisiasa zitapungua,linaandika Frankfurter Allgemeine.Vyombo vya habari mjini Tripoli,linasema gazeti hilo mashuhuri la Ujerumani,vimesherehekea uamuzi huo kuwa ni "wa kihistoria katika kuijenga Libya ya kidemokrasia.Juhudi za kuimarisha mfumo wa demokrasia zitapata nguvu uchaguzi wa bunge utakapoitishwa wiki mbili kutoka sasa linamaliza kuandika gazeti la Frankfurter Allgemeine.
Afrika Bara la Matumaini
Mada ya mwisho katika ukurasa huu wa Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii inaturejesha hapa hapa Ujerumani ambako gazeti la der Tagesspiegel linajiuliza kwanini makampuni ya Ujerumani yanabaki nyuma barani Afrika licha ya neema kubwa iliyoko barani huo?Vita,maradhi,rushwa;hiyo ndiyo picha iliyoganda vichwani wa wajasiria mali wengi wa Ujerumani wanapofikiria kuhusu bara la Afrika.Picha hiyo mbaya pengine ndio sababu kwanini biashara ya nje ya makampuni ya Ujerumani kwa bara la Afrika imetuwama katika mstari wa asili mia 2.3 na kwamba makampuni 100 yanayoendesha shughuli zake kwa sasa barani humo hayawakilishwi ipasavyo.Der Tagesspiegel linawanukuu wataalam wa kiuchumi wakisema bara la Afrika sio tu lina neema ya mali ghafi bali pia huko ndiko yatakakoibuka maeneo ya uzalishaji na soko la siku za mbele.Hadi mwaka 2020,wachunguzi wa masuala ya kiuchumi wanatarajia tabaka ya kati itaongezeka barani Afrika na kwa namna hiyo kuinua idadi ya wanunuzi.Uchunguzi uliofanywa na kuwahusisha wataalam wa kiuchumi na mameneja kutoka makampuni 15 ya magari,teknolojia ya habari na mawasiliano sawa na uhandisi umebainisha wanamkakati wanaliangalia bara la Afrika kuwa ni bara la matumaini ya ukuaji wa kiuchumi ambako makampuni ya Ujerumani yanaweza pia kufaidika-
Hadi wakati mwengine katika ukurasa kama huu,ni Oummilkheir ninaekushurukuni na kukuageni kwakherini.
Post a Comment