Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Hai,Clement Kwayu
akimzungumzia Mrembo aliyewahi kushika taji la Miss Tanzania ,Fraja Kotta
Nyalandu kuhusu kitabu chake alichozindua hivi karibuni.
|
Katika kusherehekea siku ya Mtoto wa Afrika
tarehe 16 Juni, Halmashauri ya Wilaya ya Hai, ikishirikiana na viongozi wa
serikali, UNICEF na Save the Children, imezindua Kituo cha Huduma Jumuishi,
kitakachowasaidia wanawake na watoto ambao wameathiriwa na ukatili.
“Katika kituo hiki, huduma za kuwasaidia wahanga
wa ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto ikiwa ni pamoja na huduma za
afya, msaada wa kisaikolojia, ulinzi/usalama na msaada wa kisheria vinaweza
kutolewa hapo katika eneo moja ndani ya kituo cha afya zikiwa zimeratibiwa
vizuri Zaidi,” alisema Charles Pallangyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii.
Aliongeza, “kituo hiki kitasaidia kupunguza
madhara zaidi ya ukatili kwa sababu wahanga wa ukatili wataweza kupata huduma
zote muhimu katika eneo moja na hawatakuwa na sababu ya kurudiarudia kuwaeleza
watoa huduma mbalimbali walio katika maeneo tofauti yale mambo mabaya
waliyoyapitia, au kutakiwa kwenda na kurudi kutokana na ukosefu wa uratibu na
uwezo wa watendaji wa sekta mbalimbali katika kuwahudumia wahanga wa ukatili
kwa ukamilifu.”
Mwakilishi wa UNICEF Tanzania, Dk. Jama Gulaid,
anaamini kuwa kama tukifanya kazi kwa ushirikiano na serikali na wadau wengine,
tunaweza kupata suluhu katika kumaliza ukatili dhidi ya watoto. “Ukatili dhidi
ya watoto uko kila mahali na hatuwezi kuendelea kuufumbia macho. Watoto wote
hapa Tanzania wanahaki ya kuishi na kukua katika mazingira yasiyo na ukatili.
Kama sisi sote tukifanya kazi kwa kushirikiana pamoja, sina shaka tutaweza
kumaliza ukatili dhidi ya watoto.”
Katika tukio hili huko Hai, UNICEF Tanzania
imemteua msanii mahiri wa bongo flava Ambwene Yessyah, anayejulikana zaidi kama
AY, pamoja na aliyewahi kuwa Miss Tanzania, Faraja Kotta Nyalandu kama Mabalozi
wao katika ‘Kampeni ya Tokomeza Ukatili Dhidi ya Watoto.’ Wote wameahidi
kusaidia kampeni ya ‘Kampeni ya Tokomeza Ukatili Dhidi ya Watoto’ na
wameonyesha kuhamasishwa na heshima hii waliyopewa kutoa sauti zao kutetea
ulinzi wa mtoto.
“Nimepewa heshima kubwa kwa kuteuliwa kwangu kuwa
Balozi wa UNICEF Tanzania na nitajitoa katika kutumia sauti yangu na umaarufu
wangu kusaidia kutokomeza ukatili dhidi ya watoto hapa Tanzania,” alisema AY
alipokuwa akikubali wadhifa huo.
Kwa kuwateua AY na Faraja Kotta Nyalandu kama
Mabalozi wa UNICEF Tanzania wa kampeni ya ‘Kampeni ya Tokomeza Ukatili Dhidi ya
Watoto’, UNICEF inategemea kuongeza uzito na muonekano zaidi wa suala la ulinzi
wa mtoto katika mijadala inayoendelea kuhusu ukatili dhidi ya watoto na
kuonyesha kuwa kuna suluhisho la tatizo hili.
Kama mwazo wa kazi yao katika shughuli za
UNICEF Tanzania, AY na Faraja Kotta Nyalandu walitembelea Dawati la Jinsia na
Watoto katika kituo cha Polisi cha Hai kuona wenyewe kazi inayofanywa kusaidia wanawake
na watoto waliofanyiwa au kuathiriwa na ukatili.
Utafiti juu ya Ukatili Dhidi ya Watoto,
uliozinduliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto mwaka 2011,
unaonyesha mambo yanayopelekea uhatarishi wa watoto kwenye ukatili kimwili na
kingono hapa Tanzania – wastani wa msichana 1 kati ya 3 na mvulana 1 kati ya 7
wamefanyiwa vitendo vya ukatili wa kingono, na zaidi ya asilimia 70 ya
wasichana na wavulana wamefanyiwa vitendo vya ukatili wa kimwili kabla
hawajafikia umri wa miaka 18. Hata hivyo, wahanga wengi hawajamwambia mtu
yeyote ukatili waliofanyiwa na ni kesi chache sana zimefikishwa polisi.
Kumekuwa na maendeleo katika kuboresha hali hii.
UNICEF inasaidia serikali ya Tanzania kupitia Idara ya Ustawi wa Jamii
kuanzisha na kuboresha ‘mifumo ya Ulinzi wa Mtoto’ katika halmashauri 13.
Katika halmashauri hizi, afya, ustawi wa jamii,
polisi, sekta za elimu na mahakama, magereza, wanasheria, asasi za kiraia
pamoja na mifumo ya kijamii isiyo rasmi wanaunda Timu ya Halmashauri ya Ulinzi
na Usalama wa Mtoto na wanashirikiana kuhakikisha kuwa kesi za ukatili wa
watoto zinashughulikiwa vyema na pia wanazuia ukatili kwa kuongeza uelewa wa
jamii juu ya ukatili dhidi ya watoto.
Lengo la Idara ya Ustawi wa Jamii ni kupanua
utaratibu wa mfumo huu katika halmashauri 30 ifikapo mwaka 2016.
Na Dixon Busagaga wa globu ya jamii kanda ya
kaskazini
Posted
by Dominic Deusdedith
|
Post a Comment